.

CHF Iliyoboreshwa

Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ulianzishwa na Serikali ya Tanzania kwa sheria ya mwaka 2001; ambapo kila Halmashauri ilitakiwa kuanzisha Mfuko wa CHF. Tathmini ya uendeshaji wa mfuko huu imeonesha kwamba utekelezaji wake unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinatokana na matatizo ya muundo na mfumo wa uendeshaji wake; matokeo yake kumekuwa na mafanikio tofauti baina ya Halmashauri moja na nyingine.

Kufuatia changamoto hizo Serikali imedhamiria kufanya maboresho katika maeneo matatu ili kuimarisha uendeshaji wa Mfuko wa Afya ya Jamii. Maeneo hayo ni;Usimamizi na Uendeshaji (Governance),Usajili wa wanachama wa Mfuko (Enrolment), Kitita cha mafao na ngazi ya upatikanaji wa huduma za Afya (Benefit Package).

Moja ya vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata matibabu kupitia mifumo ya bima za afya hasa wananchi walioko katika sekta isiyokuwa rasmi ili kufikia lengo la afya bora kwa wote, pia kusimamia ukusanyaji / upatikanaji wa fedha, kutoa huduma zilizo bora zenye gharama nafuu na Kuboresha huduma za afya katika jamii.

Ili kufanikisha azma hiyo Ofisi ya Raisi - TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imefanya maboresho mbalimbali kwa kuleta mfumo mpya wa CHF iliyoboreshwa, ambao unatekelezwa kwa kupitia 'Waraka Namba 1 wa Maboresho ya Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF/TIKA) lengo ni kuleta tija na ufanisi katika uratibu na utoaji wa huduma ya mfuko wa Afya ya Jamii ili hatimae kufikia malengo ya Kitaifa.